Thursday, December 18, 2008

Wakili ashinda kura za maoni Chadema Mbeya Vijijini


2008-12-18 12:33:47 Na Thobias Mwanakatwe, Mbeya
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimekamilisha mchakato wa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini unaotarajia kufanyika Januari 25, mwakani. Uchaguzi huo unafuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Richard Said Nyaulawa, aliyefariki dunia mwezi uliopita kutokana na ugonjwa wa kansa ya ini. Jana, Mkutano wa Chadema wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, ulimchagua wakili wa kujitegemea, Sambwee Shitambala, kuwania ubunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini kupitia chama hicho. Shitambala aliibuka mshindi katika mkutano wa kura za maoni uliofanyika katika Hoteli ya Tughimbe mjini Mbalizi kwa kupata kura 44 na kuwashinda washindani wake watatu. Wagombea walioangushwa katika kinyang`anyiro hicho ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Mbeya Vijijini, Ipyana Seme aliyeambulia kura 18, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nswila, Amos Nsote aliyepata kura 17 na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu (Duce), Burton Gwakisa, aliambulia kura saba. Kufuatia matokeo hayo, Shitambala, anasubiri kuidhinishwa na Kamati Kuu ya Chadema itakayokutana mjini Mbalizi ambapo viongozi wakuu wa chama hicho, Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk.Wilbroad Slaa watahudhuria. Akizungumza na Nipashe baada ya kutangazwa mshindi, Shitambala ambaye alipata Shahada ya Uzamili ya Sheria nchini Uingereza, alisema kwake siasa siyo ajira bali ni huduma kwa jamii. Alisema kama atachaguliwa na wananchi wa Jimbo la Mbeya Vijijini atahakikisha anatumia taaluma yake ya sheria kwa kuwasaidia kuwaelimisha wananchi elimu ya uraia ili wajue wajibu wao na kuzifahamu haki zao za msingi. Alisema zipo baadhi ya sheria ambazo bado ni kandamizi kwa jamii hivyo atakapoingia bungeni atasaidia kuzipigia kelele ili zirekebishwe. Wakati huo huo, wanachama wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) wamejitokeza kuchukua fomu, akiwemo Askofu wa Kanisa la Pentekoste, ili kugombea ubunge wa jimbo hilo. Katibu wa CUF Mbeya Vijijini, Ernest Gunza, akizungumza na Nipashe alisema miongoni mwa wanachama waliochukua fomu za kuwania ubunge ni Askofu wa Kanisa la Pentekoste PCG Mbeya, Samson Mwalyego, na mfanyabiashara wa mji wa Mbalizi, Obadia Nkyenky. Alisema zoezi la kuchukua fomu bado linaendelea hadi kesho. Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, ZittoKabwe, amesema chama chake hakipingi ushirikiano wa vyama vya upinzani katika kumweka mgombea mmoja kwenye uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Vijijini.

No comments: