Thursday, December 4, 2008

RC Mbeya amtimua Mkurugenzi

RC Mbeya amtimua Mkurugenzi
na Christopher Nyenyembe, MbeyaMKUU wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, katika hali iliyoonyesha kutoridhishwa na utendaji wa kazi wa Mkurugenzi wa jiji hilo, Elizabeth Munuo, amemwamuru aondoke kwenda kutafuta kazi nyingine kama kazi aliyonayo imemshinda.Mwakipesile alitoa kauli hiyo jana mara baada ya Munuo kulalama katika kikao cha bodi ya barabara kilichokutana mjini hapa kuwa anajuta na kujilaumu kuhamishiwa Jiji la Mbeya, lenye uchafu uliokithiri na lisilo na vitendea kazi.Munuo alitoa kauli hiyo alipotakiwa na wajumbe kuelezea mikakati ya kukabiliana na tatizo la uchafu katika jiji hilo, ambalo limekithiri kwa uchafu kila kona na kwenye lango kuu la kuingilia eneo la Uyole ambako kuna dampo kubwa la kutupia taka, lakini zinamwagwa taka hadi barabarani.Huku akisikilizwa kwa makini na wajumbe hao, mkurugenzi huyo badala ya kuelezea mikakati yake, alijikuta akiweka wazi uchungu alionao wa kujutia uamuzi wa serikali wa kumhamishia hapo, huku akidai kuwa mikoa aliyotoka haikuwa hivyo.“Hapa kwenu Mbeya, nilipokuja nilikuta hakuna wahisani, nasikia waliondoka baada ya kusumbuliwa na matukio ya ujambazi, nilikuta halmashauri ikiwa katika hali hiyo na tumeendelea hivyo hivyo na magari mawili ya kuzolea taka, bajeti ya mwaka huu tumeweka magari mawili ya taka angalau yatusaidie lakini jiji hili linahitaji magari 10,” alisema Munuo.Munuo alikiri kuwa jiji hilo limekithiri kwa uchafu ambao hauwezi kuondolewa kwa kutumia magari mawili, tena mabovu na kwamba ukosefu wa magari mapya umetokana na tatizo lililowaondoa wahisani.“Hata mimi mwenyewe najilaumu ilikuwaje nikahamishiwa katika mji huu waliofukuzwa wahisani na nimekuta hali chafu, miji yote niliyokaa ilikuwa na hali nzuri, si Mbeya ndugu mwenyekiti,” alisema mkurugenzi huyo.Ndipo Mkuu wa mkoa huo, Mwakipesile akionyesha wazi kuchukizwa na kauli ya mkurugenzi huyo ya kuubeza uamuzi wa serikali wa kumhamishia kwenye jiji hilo, aligonga meza na kumpasha kuwa kama ameshindwa kazi aondoke.“Kama huwezi kazi nenda, go goo, ondoka, katafute kazi sehemu nyingine, Where you think you can do a better job, go, go hatuwezi kufanya kazi kwa kubembelezana, go nenda, takataka zinatupwa hadi barabarani unatuletea utetezi hata mifereji mnashindwa kuzibua, no,” alisema Mwakipesile kwa ukali.Mbali ya mkuu wa mkoa huyo, kauli hiyo pia iliwafanya wajumbe wengine wa kikao hicho akiwemo Mbunge wa Viti Maalumu, Hilda Ngoye, ambaye alitahadharisha kuwa uchafu wa jiji hilo haupaswi kufumbiwa macho kwani unaweza kuwa chimbuko la matatizo mengi.Aliyefuatia alikuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Benson Mpesya, ambaye hakuridhishwa na hoja ya ukosefu wa vifaa vya usafi, isipokuwa alidai kuwa watendaji wa halmashauri hiyo hawajajipanga kukabiliana na tatizo hilo, hivyo kusababisha takataka zizagae kila kona.Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, alisema inatia shaka kwa mtendaji wa serikali kudai kuwa kule alikokuwa, kulikuwa kusafi kuliko Jiji la Mbeya alikohamishiwa kwani hali hiyo inaonyesha upungufu wa uwajibikaji.“Hii ni changamoto kwako mkuu wa mkoa, kwa kuwa watu hawa unaishi nao kila siku na hali ya uchafu unaiona, ulichopaswa ni kutoa maagizo ya jiji liwe safi, unakumbuka Jiji la Dar es Salaam liliwahi kuvunjwa na kuwa mamlaka, sasa hatuoni sababu ya utetezi huu unaotolewa hapa wa kujutia kuhamishiwa Mbeya, ” alisema Zambi.Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, alimuomba, mkuu wa mkoa huo amtake mkurugenzi huyo afute kauli yake, kwa madai kuwa inadhalilisha utendaji mzima wa serikali katika jiji hilo.Mstahiki Meya wa jiji hilo, Athanas Kapunga, aliingilia kati kwa kukiri upungufu wa kuwapo kwa uchafu katika jiji leo.Alisema yote yaliyosemwa na wajumbe katika kikao hicho, yatazungumzwa na madiwani wa halmashauri hiyo, huku akielezea wazi kuwa mji huo umekuwa ukiendelea kushuka hadhi tofauti na miaka ya nyuma.Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen, alilitaka jiji hilo kuhakikisha linaweka taa za barabarani kama urembo, lakini zitakuwa sehemu muhimu ya ulinzi kwa kupunguza vitendo vya uhalifu.“Mimi sitaki kujikita huko kwenye uchafu, mimi nahamia upande wa taa za barabarani, kwetu sisi taa ni ulinzi mkubwa, zinasaidia kupunguza upigaji wa nondo, hii inatia aibu badala ya Mbeya kuwa jiji, linakuwa zizi,” alisema Kamanda Stephen. Tanzania Daima

No comments: