Monday, December 15, 2008

Harakati za Uchaguzi Mbeya Vijijini!




Wapinzani sasa wasambaratika Mbeya Vijijini 2008-12-15 12:56:43 Na Joseph Mwendapole na Muhibu Said
Kambi ya upinzani, imeshindwa tena kuungana na kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Mbeya Vijijini. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Januari 25, mwakani. Jimbo hilo liko wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wake, Richard Nyaulawa (CCM) kufariki dunia. Vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF, vilianzisha ushirikiano ambapo vilikubaliana kuwa vitasimamisha mgombea mmoja katika chaguzi pale ambapo itaonekana chama kimojawapo kinaungwa mkono pamoja na kuwa na msimamo mmoja katika masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Ushirikiano huo uliingia doa Oktoba, mwaka huu katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani katika kata ya Tarime Mjini na jimbo la Tarime wa kujaza nafasi hizo kufuatia kifo cha aliyekuwa anazishikilia, Chacha Zakayo Wangwe kufariki dunia. Katika uchaguzi huo, kambi ya upinzani ilishindwa kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja hivyo Chadema, NCCR-Mageuzi kila kimoja zikasimamisha wagombea huku TLP ikikiunga mkono NCCR-Mageuzi na CUF kukiunga mkono Chadema. Democrat (DP) ambacho hakiko katika ushirikiano huo nacho kilisimamisha wagombea. Mwenyekiti wa DP, Christopher Mtikila, alisema jana kuwa chama chake kiko katika mchakato wa kumpata mgombea atakayesimamishwa kuwania jimbo hilo. Alisema wanatarajia mchakato huo utakamilika na hatimaye mgombea kupatikana wiki hii. Kwa upande wake, Chadema) kimesema kinatarajia kusimamisha mgombea na tayari mchakato umeanza. Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Willbroad Slaa, alisema uteuzi wa Wilaya utafanyika Desemba 17 na Kamati Kuu ya chama itakaa Desemba 20. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, alisema jana kuwa hajajua iwapo chama chake kitasimamisha mgombea au la. ``Nipe muda wa saa moja kisha nitakujibu kama tutasimamisha mgombea au la, ngoja niwasiliane na wenzangu ntakujulisha,`` alisema Mrema. Hata hivyo, gazeti hili lilipowasiliana naye baada ya muda huo Mrema hakupokea simu licha ya kupigiwa mara kwa mara. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba, alisema Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, ndiye atakayekuwa msimamizi wa mchakato mzima kwa upande wa kwa CUF katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini. Alisema CUF kilimwandikia barua Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ili chama hicho kikiunge mkono CUF katika uchaguzi huo lakini hadi jana Mbowe hakuwa ameijibu barua hiyo. Profesa Lipumba alisema CUF kitashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na wana matumaini ya kushinda kwa kuwa mgombea wao katika uchaguzi wa mwaka 2005 alishika nafasi ya pili nyuma ya marehemu Nyaulawa. Alisema ushirikiano wa kisiasa wa vyama vinne una mtihani mgumu kwa kuwa baadhi ya vyama vimeonyesha dalili zote za kudhoofika. Akizungumza na Nipashe jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini, alisema wanasubiri uamuzi wa vikao vya juu vya chama hicho vitakavyoamua iwapo chama hicho kisimamishe mgombea au la. Alisema ingawa wana nia ya kumsimamisha mgombea wao, lakini kwanza watapima upepo kabla yakufikia uamuzi huo. Selasini alisema yeye alikuwa Mbeya kwa wiki tatu kufanya tathmini ya kisiasa na aliyoyaona huko yatawasilishwa kwenye vikao vya ngazi za juu ili yafanyiwe maamuzi. Mchakato wa uchaguzi huo mdogo umeashaanza rasmi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa ratiba yake inayoonyesha kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika Desemba 27 wakati kampeni zitaanza rasmi Desemba 28 hadi Januari 24, siku moja kabla ya upigaji kura. Uamuzi wa kila chama kusimamisha mgombea wake unakipa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nafasi nzuri ya kushinda kutokana na kambi ya upinzani kugawana kura.

No comments: