http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?id=14560
Habari za Kitaifa
Habari zaidi!
Jenerali Mboma ajitosa kuwania kiti cha Mbeya Vijijini
Merali Chawe, MbeyaDaily News; Friday,December 12, 2008 @21:15
Habari nyingine
Wanafunzi vyuo vikuu waaswa kujaza fomu za kurejea darasani
Jenerali Mboma ajitosa kuwania kiti cha Mbeya Vijijini
Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Robert Mboma jana alikuwa mwana-CCM wa tisa kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa kuwania nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini na kumaliza uvumi uliokuwa umetawala kama atajitosa katika kinyang'anyiro hicho ama la. Kuingia kwa Jenerali Mboma katika kinyang'anyiro hicho ndani ya CCM kumebadili mwelekeo na kusababisha wanachama waliochukuwa fomu kuwania nafasi hiyo huku wakiwa na imani ya kuibuka na ushindi kuanza kupigana vijembe wao wenyewe. Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kuchukua fomu, Mbona alipinga madai yanayotolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa mstaafu huyo wa Jeshi ametumwa na Rais Jakaya Kikwete kuja kugombea katika jimbo hilo lililoachwa wazi na Richard Nyaulawa. "Mimi napiga vita sana kupigana vijembe, na hii ndio dalili yenyewe ya kupigana vijembe, Rais Kikwete kamwe hawezi kufanya kitu kama hicho," alisema na kuongeza kuwa ameamua kuingia katika kinyang'anyiro hicho kwa utashi wake mwenyewe. Aidha alisema ameamua kuingia katika ulingo wa siasa si kwa ajili ya kutafuta maslahi, lakini kwa sababu anataka kutatua kero zinazowakabili wananchi hususani suala la mbolea, umeme na maji, mambo ambayo yanakwamisha shughuli za kiuchumi za wananchi wa jimbo hilo. Alisema kuwa kabla ya siasa kutenganishwa na Jeshi alifanikiwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM na kwamba ana uzoefu na masuala ya siasa na kwamba ana imani akishinda ataweza kutatua kero mbalimbali za wananchi. Hadi kufikia jana mchana, wanaCCM tisa walikuwa wamechukua fomu za kuomba kuwania nafasi ya ubunge wa jimbo hilo, mbali ya Jenerali Mboma wengine ni Allan Mwaigaga, Djovita Diyami, Maiko Mponzi, Flora Mwalyambi, Petro Mwashusya, Mchungaji Luckson Mwanjali, Mariam Mwambanga na Andrew Sayila. Mwisho wa kuchukua fomu kwa wanaowania kuteuliwa na CCM ni leo saa 10 alasiri, ambapo kampeni za uchaguzi wa jimbo hilo zinatarajiwa kuanza Desemba 27 na uchaguzi unatarajia kufanyika Januari 25, mwakani. Wakati CCM leo ikikamilisha shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu kwa wanachama wake, Chadema bado inaendelea na mchakato wa utoaji fomu utakaofikia tamati Desemba 15, ambapo kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), tayari kimemtangaza Mwanamama Amina Ahmed kugombea katika jimbo hilo.
A day in the life...
7 years ago
No comments:
Post a Comment