Sunday, December 28, 2008

Ubunge Mbeya Vijijini


http://www.mwananchi.co.tz/newsrids.asp?id=8868
Mambo ya Harakati za Ubunge Mbeya Vijijini.
Urejeshaji fomu wafunika Mbeya Vijijini
Na Brandy Nelson, Mbeya
SHAMRASHAMRA na chereko jana ziliifunika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbeya vijijini kutokana na mashabiki wa vyama kuwasikidikiza wagombea wao kurejesha fomu kwa maandamano.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ndio waliokuwa wa kwanza kurejesha fomu huku mgombea wao Sambwee Shitambala akisindikizwa na mamia ya wafuasi wa chama hicho waliokuwa wakiimba nyingi za kejeli dhidi ya Chama cha Mapinduzi.
Huku wengine wakiimba, CCM fisadi, CCM fisadi, wengine walikuwa wamebeba bendera za chama hicho wakiwa na magari, baskeli na pikipiki.
Katika ofisi hizo wafuasi wa Chadema kutoka katika
maeneo mbalimbali ya Mbeya Vijijini waliotembea kwa mguu kutoka katika ofisi za chama hicho zilizoko maeneo ya Mama John kwa maandamano, walijazana wakishuhudia mgombea wao akirejesha fomu.
Kwa upande wake CCM, walianza maadamano yao Mbeya Vijijini mapema asubuhi wakiwa na magari yaliyojaa wapambe huku mgombea wao, Lackson Mwanjali akiwa juu ya gari akipungia mkono watu waliokuwa pembeni ya barabara.
Hata hivyo, msafara wake ulipata msukosuko alipofika katika eneo la Stendi na Soko la Mbalizi Mbeya vijijini alipokutana na watu waliomzomea.
Katika hali isiyo ya kawaida wananchi na waliokuwa pembezoni mwa barabara walionekana ni wafuasi wa vyama vingine waliuzomea msafara huo huku wakipiga kelele za mafisadi , mafisadi na kusababisha mgombea huyo kukerwa na hali hiyo.
Baada ya kuonekana makelele yanazidi aliamua kuwapa ishara kwa kunyosha vidole viwili juu vya mkono wa kushoto na kimoja cha mkono wa kulia kupachika katikati ya vidole hivyo.
Hali hiyo ilisababisha mji mdogo wa Mbalizi kuzidi kwa makelele na kumzomea, hali ambayo iliulazimu msafara wake kusitisha maadamano na kurejesha fomu kimya kimya.
Akizungumza baada ya kurudisha fomu zilizopokelewa na Msimamizi wa Uchaguzi, Juliana Malange, mgombea wa Chadema, Sambwee Shitambala alisema ameamua kugombea uongozi katika jimbo hilo ili kudhihirisha kuwa wananchi wa jimbo hilo wanataka maendeleo.
Shitambala alisema wakati wa mabadiliko umefika sasa na kuwaahidi wananchi wa jimbo hilo kuwa hajagombea ili awe mtawala bali amekuja kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo waliozingirwa na umasikini tangu nchi hii ilipopata uhuru miaka 45 iliyopita.
Wengine waliorudisha fomu ni pamoja Subi Mwakapiki wa Chama cha Sauti ya Umma na Daud Mponzi wa Chama cha wananachi (CUF).
Kampeni za uchaguzi huo wa kuziba nafasi iliyoachwa kufuatia kifo cha mbunge wa jimbo hilo, Richard Nyaulawa, zinatarajiwa kuanza Desemba 30 mwaka huu.
Wakati huo huo, Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Mwamboma amekihama chama hicho na kujiunga na Chadema.
Mwamboma ni miongoni mwa wananchi wengine 102 wa vijiji vya Itewe, Inyala na Idunda vilivyopo katika kata ya Inyala Wilaya ya Mbeya vijijini waliorudisha kadi za CCM na kujiunga na Chadema huku wadai kuhama kwa sababu chama hicho kimewatelekeza tangu walipokichagua mwaka 2005.
Mwamboma aliyekuwa na kadi ya CCM namba 177601 iliyotolewa Julai 22 mwaka 2003, alichukua kadi ya Chadema yenye namba 0139981 ambayo alikabidhiwa na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Said Arfi.
Alisema kuwa kuwa ameamua kwa hiari yake kujiunga na Chadema kutokana kuonesha muelekeo wa maendeleo wenye nia ya kulikomboa jimbo hilo na kuleta maendeleo ya kiuchumi.
"Kama kijana nilikuwa na matumaini kwamba CCM itawavusha na kuwakwamua kiuchumi lakini matokeo yake viongozi wakuu wa serikali wameonekana wazi wakituhumiwa kwa ufisadi na ulaji wa rushwa, jambo ambalo limenifanya nikose
imani na chama hicho," alisema
Wanachama hao walisema kuwa viongozi wa CCM walifika hapo wa kampeni za uchaguzi mwaka 2005 na kuwagawia nguo, kofia na kanga na baada ya hapo hawajarudi tena kijijini
hapo.
"Kitendo kilichofanywa na viongozi wa CCM kimesababisha tukione chama hicho hakina nia ya kutekeleza ahadi walizotuahidi wakati wa kampeni, hivyo tumeamua kukiacha na kujiunga na Chadema na ndiyo mkombozi wetu," alisema.

No comments: