Tuesday, January 6, 2009

Chifu ataka CCM isichaguliwe Mbeya

Chifu ataka CCM isichaguliwe Mbeya
Na Brandy Nelson, Mbeya
CHIFU mkuu wa kabila la Wamalila, lililo katika tarafa ya Isangati wilayani Mbeya Vijijini, Golian Mpoli, 90, amewataka wananchi wake kutokichagua chama
ambacho kinawanyima maendeleo na badala yake wamsubiri mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Sambwee Shitambala, katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Mgombea huyo alienguliwa kwenye kinyang'anyiro cha kiti cha ubunge cha jimbo la Mbeya Vijijini baada ya kugundulika kwa kasoro kwenye kiapo chake. Vyama vya CCM na CUF vilibaini kasoro hizo na kuweka pingamizi ambalo lilikubaliwa na Tume ya Uchaguzi.
Lakini chifu huyo wa kabila la Wamalila anaona kuwa bado kuna haja ya kumsubiri mgombea huyo katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa hawana la kufanya kwa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Chifu Mpoli, akiwa na mkalimani kutokana na kutojua vizuri lugha ya Kiswahili, alisema kuwa toka uhuru wamekuwa wakitawaliwa na viongozi wa CCM, lakini hakuna maendeleo yoyote ambayo chama hicho kimewapa zaidi ya kuendelea kuwanyonya.
Alipoulizwa kuwa ni kwanini anamtaka Sambwee Shitambala kuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini wakati hajawahi hata kuwaongoza na pia si mzaliwa wa tarafa hiyo ya Isangati, Chifu Mpoli alisema kuwa kutokana na jinsi alivyomuona na kutafakari anaamini anaweza kuwasaidia wananchi wake.
"Tangu afariki mbunge wetu Edward Shiwa aliyetuongoza kipindi cha mwaka 1995 hadi 2000, tulikuwa hatuna shida yoyote kwa kuwa alikuwa anatusikiliza na kutatua shida zetu na alianza harakati za kuleta umeme. Alifikia hatua ya kuwekwa nguzo na bahati mbaya akafariki dunia kabla ya kulimalizia," alisema.
Alisema tangu alipoondoka mbunge huyo bado nguzo hizo zimelazwa chini na
nyingine zimechimbiwa, lakini hakuna maendeleo yoyote ya suala la kupata umeme kwa wananchi wa tarafa hiyo.
Chifu huyo alisema kuwa Mbunge Shiwa ndiye aliwaletea wazo la kujenga Shule ya Sekondari ya Ilembo na kwamba baada ya hapo tangu mwaka juzi wamekuwa wakichangishwa fedha kila mara kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, lakini hakuna kinachoendelea.
"Baada ya kuondoka Mbunge Shiwa, kuna wabunge wa CCM walikuwepo lakini hakuna walilotufanyia kama huyu wa mwisho... pamoja na kuwa mimi ni chifu mkuu nilikuwa simfahamu... nilikuwa nasikia jina tu mpaka alipofariki dunia. Hivyo kwa niaba ya machifu wenzangu na wananchi, hatuitaki CCM... tunamsubiria Sambwee Shitambala mwaka ujao, ndiyo maana nimeamu kuja huku kuwaeleza," alisema.
Alipoulizwa sababu za kutoitaka CCM, chifu huyo alijibu kuwa viongozi wake wanawanyonya wananchi na wamekuwa na matatizo mengi katika eneo hilo lakini viongozi wa CCM wanashindwa kutatua na kwamba tayari kikao cha machifu kimefanyika katika kujadili suala hilo na kwamba wamekubalina wamsubiri Shitambala mwaka 2010 ili aweze kuwasaidia katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Wakiongea na Mwananchi, baadhi ya wananchi wa kata ya Ilembo walisema kuwa kitendo cha kuondolewa mgombea wa Chadema ni sawa na kunyang`anywa tonge la ugali mdomoni kwa kuwa hali hiyo imewasikitisha sana.
Walisema kuwa kati ya wabunge watatu waliowahi kuongoza jimbo la Mbeya Vijijini, ni Shiwa (CCM) ndiye aliyeweza kuwaletea maendeleo hivyo bado anahitaji mabadiliko na kwamba msimamo wao ni kuchagua chama pinzani.
"Kama Mbunge Yete Mwaliyego ambaye alichaguliwa mwaka 2000 huyo ndiyo hatusemi kwani alikuwa anaomba kura kwa mabavu na alifikia hata kutuambia kuwa mnichague msinichague mimi ni mbunge wenu tu na alipochaguliwa hakuonekana tena hadi naye alipofariki dunia," alisema Sipiti Solomoni wa Kijiji cha Ilembo.
Alisema kuwa wao ni wanachama wa CCM na wana kadi za CCM, lakini dhamira yao ilikuwa ni kumchagua mgombea wa Chadema kwa kuwa ndiye alikuwa chaguo lao hivyo kwa sasa hawana la kufanya.
"Kweli suala la mgombea wa Chaema kuondolewa limetuumiza sana tulikuwa tunampenda na bado tunampenda na tunamuhitaji awe mbunge wetu kwani ndiye tuliyemdhania kuwa angeleta mabadiliko katika jimbo hili... labda kama anaweza kupita huyo wa CCM wakimchagua kwani anasema kwa yeye katumwa na Mungu aje kuwa mbunge," alisema.
Walisema kuwa wanahitaji mabadiliko kwani CCM imekuwa ikiwahaidi lakini hakuna mafanikio yoyote na kwamba wamechoka na chama hicho ambcho wamekuwa wasikilza kiula mara sera zake lakini hakuna zinazotekelezwa katika eneo hilo.
"Msimamo wetu ni ule ule wa kutaka mbunge kutoka katika chama cha upinzani. CUF wamekuja hapa tumewasikiliza sera zao na tunawasubiri kuona sera zao ni nini kama tunaona nao hawaturidhishi, basi tutajua la kufanya," alisema mmoja wao.
Wananchi hao ambao walikuta wamesimama katika vikundi vikundi maeneo ya klabu cha pombe na sokoni katika kijiji hicho cha Ilembo ambacho rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alizindua kampeni za CCM.
Walipohojiwa kama wangeenda kwenye mkutano huo wa uzinduzi, walisema kuwa wangeenda kwa ajili kumfahamu rais huyo mstaafu kwa kuwa hawajawahi kumuona.

No comments: