Saturday, January 3, 2009

CHADEMA Walizwa na NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetupilia mbali rufani ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Sambwee Shitambala, dhidi ya uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kumwondoa katika orodha ya wanaowania ubunge kwenye uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini. Shitambala ambaye aliwasilisha rufani dhidi ya uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Desemba 30, mwaka jana baada ya kuwekewa pingamizi na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), kwamba alikiuka taratibu za ujazaji fomu hiyo, kwa kuapa kwa kutumia wakili badala ya mahakama kama sheria ya uchaguzi inavyoagiza. Akitolea uamuzi wa rafani hiyo Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Lewis Makame, alisema Tume ilimwita mrufani juzi kwa lengo la kupata maelezo ya ziada kuhusu sababu za rufani aliyowasilisha na kwamba, hayakupishana na yaliyoandikwa. Jaji Makame alisema kwa kuzingatia sababu za rufani, NEC iliona hoja tatu za msingi zilizokuwemo ambazo ni Je, tamko la kisheria lililotolewa na mrufani katika fomu zake za uteuzi ni halali kwa mujibu wa kifungu cha 38(3) (a) cha Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985? Je, Sheria ya Viapo (The Oath and Statutory Declarations Act (CAP 34 R. E. 2002) na Sheria ya Wanaoidhinisha Viapo (The Notaries Public and Commissiners for Oaths Act (CAP 12 R.E. 2002) zinaweza kutumika katika suala hili? Alisema tatu,Tume iliangalia hoja ambayo wagombea walikuwa na muda wa kutosha wa kukamilisha fomu zao za uteuzi na kuziwasilisha kwa wakati? Aidha, Je,Tume inaweza kutumia ``proviso`` ya kifungu cha 38(4) cha Sheria ya Uchaguzi na. 1 ya mwaka 1985? Alifafanua kuwa baada ya kuzipitia hoja hizo za msingi, NEC ilibaini kuwa mgombea wa Chadema alikiuka taratibu ya kula kiapo kwa wakili aliyemtaja kwa jina la Evarist Martin Mashiba wa S L P 4185 Dar es Salaam na kugongwa muhuri wa wakili huyo na kwamba, kifungu cha 38(3) (a) cha Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 kimebainisha tamko linalotakiwa kufanywa na mgombea ubunge. ``Kila fomu ya mgombea uchaguzi lazima iambatane na tamko rasmi la kisheria ambalo limewekwa saini na mgombea mbele ya hakimu likitamka bayana sifa za mgombea na vile vile kutamka wazi kuwa mgombea hana pingamizi kugombea katika uchaguzi,`` alisema. Alisema hivyo katika kifungu hicho neno ``shall`` ndio lililotumika ambalo linaonyesha ni �lazima� mgombea kula kiapo mahakamani na kwa Hakimu Mkazi, Wilaya na Mahakama za Mwanzo hivyo ni dhahiri kwamba, wakili hapaswi kushuhudia tamko husika na tamko hilo litakuwa sio halali. Aliendelea kuwa kipengele cha Sheria za Viapo na Sheria ya Wanaoidhinisha Viapo, hakiwezi kutumika katika suala hilo kwa sababu Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 imetamka bayana kuhusu anayetakiwa kushuhudia tamko la kisheria la mgombea. Jaji Makame alisema NEC ilitangaza Desemba 17, wagombea kuchukua fomu na kurudisha Desemba 27, kwa maana hiyo kulikuwa na siku sita za kazi hivyo mahakama zilikuwa zinafanya kazi na wagombea walipaswa kutumia siku hizo kula kiapo kwa hakimu. Pia, Tume hiyo imeridhika na maelezo ya mrufani kuwa hakujiapisha mwenyewe na wala hajaajiriwa na Kampuni ya Evarist Mashiba Advocates kama ilivyodaiwa na mweka pingamizi. Kwa upande wa mgombea wa DP, naye amegonga mwamba rufani yake kama sababu za mgombea wa Chadema. Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mbunge wa Mpanda Kati, Saidi Arfi, alisema chama kitakaa chini kutafakari uamuzi uliotolewa na Tume kwa sababu, ni pigo kwa demokrasia nchini. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, alisema hivi sasa bado hawajaamua kuunga mkono CUF. ``Kwa kuwa jambo lenyewe limetokea sasa, tutakaa na kisha baadaye kutoa taarifa kamili kwa umma, kwa sasa bado tunatafakari,`` alisema Slaa. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Januari 25, unafuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Vijijini, Richard Nyaulawa (CCM).

No comments: