Friday, January 2, 2009

Mambo ya Mbeya Vijijini na Uchaguzi wa MP


Date::1/2/2009
Mambo magumu Mbeya Vijijini
*Hatima ya mgombea Chadema leo
Na Brandy Nelson, Mbeya
MAMBO yanazidi kuwa magumu katika mchakato wa uchaguzi mdogo wa mbunge Mbeya Vijijini baada ya kuzidi kwa matukio yanayopandisha joto zaidi la kisiasa mkoani Mbeya na hata maeneo mengine ya nchi.
Kuahirishwa kutangazwa kwa matokeo ya rufaa ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Sambwee Shitambala, hadi leo asubuhi, kumelimepandisha joto kwenye kinyang'anyiro cha kuziba nafasi iliyoachwa na mbunge wa CCM, Richard Nyaulawa.
Awali ilitaarifiwa kuwa uamuzi wa rufaa ya Shitambala, ambaye alienguliwa kugombea ubunge wa Mbeya Vijijini kwa kuapa kwa wakili badala ya hakimu, ingetolewa jana saa 4:00 asubuhi.
Lakini mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Lewis Makame aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa majibu ya rufaa yatatolewa leo saa 5:00 asubuhi wakati yale ya mgombea wa DP, Ndele Mboma yatatolewa saa 8:00 mchana.
Aliyasema hayo jana majira ya saa 10:00 jioni baada ya wagombea, walioenguliwa na msimamizi wa uchaguzi katika kinayang'anyiro cha ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini na baadaye kukata rufaa, kuhojiwa na tume yake kwenye hoteli ya Mount Livingstone.
"Tumeshapitia rufaa za wagombea wote na majibu tutayatoa kesho saa 5:00 asubuhi kwa mgombea wa Chadema Sambwee Shitambala na saa 8:00 kwa mgombea wa DP, Ndele Mboma," alisema.
Aidha tume hiyo imeagiza wagombea hao wasiendelee na mikutano ya kampeni za uchaguzi, ikibatilisha uamuzi wa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Vijijini, Juliana Malange, ambaye aliwaruhusu kufanya kampeni wakati wakisubiri majibu ya rufaa zao.
Mgombea wa Chadema alifanya mkutano wa kampeni juzi katika kata ya Utengule, Usongwe.
Akiongea baada ya kutoka kuhojiwa, Shitambala alisema kuwa alipata nafasi ya kutoa maelezo mengi kulingana na kosa lililosababisha aenguliwe katika uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na sheria inavyoelekeza katika masuala ya utoaji wa kiapo.
"Pia wametuhoji kuwa wamesikia kwamba tulifanya mkutano wa kampeni, tukamjibu ndiyo kwa kuwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Vijijini alituruhusu kuendelea na kampeni," alisema na kuongeza kuwa maamuzi hayo yalikuwa sahihi.
Shitambala alisema kuwa pamoja na maelezo hayo tume imewataka kutoendelea na kampeni hadi baada ya uamuzi kutangazwa kesho.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinadai kuwa wajumbe wa tume hiyo, walianza mjadala wa rufaa hiyo mara baada ya kuwasili hotelini hapo saa 4:00 na kwamba, kulikuwa na mvutano mkubwa hadi majira ya saa 7:00 usiku wa kuamkia jana.
Inadaiwa kikao hicho kiliendelea tena jana asubuhi hadi saa 9:00 wakati walipowaita wagombea na kuwahoji na kumaliza saa 10:00 jioni.

No comments: